Mawakili maarufu nchini Tundu Lissu na Godfrey Wasonga jana nusura wazipige kavukavu na kama si busara za mawakili wengine waliokuwa wamefurika katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma na hasa Deus Nyabiri, huenda hali ingekuwa tofauti.
Katika mahakama hiyo, ambayo ilifurika umati mkubwa wa mawakili na wasikilizaji, wawili hao waliibua mzozo wakiwa kwenye korido walipokuwa wakisubiri kuingia kwenye chumba cha mahakama kuanza kusikilizwa kwa kesi mbili, ya kwanza namba 12/2017 ya kupinga uchaguzi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) ambayo ilifunguliwa na Wasonga, na nyingine ni namba 13 na 14/2017 ambazo Lissu na wenzake walipeleka maombi ya kuunganishwa katika kesi hiyo ya Wasonga.
Sakata lilianzia kwa Lissu, ambaye aliwashawishi wenzake kumuunga mkono kabla ya kuanza kesi hiyo kuwa wamuombe Jaji Awadh Muhamed abadilishe chumba cha kusikilizia kesi hizo kutokana na umati uliokuwa umefurika akisema eneo alilopanga lilikuwa ni dogo.
Hoja hiyo ilipingwa na Wasonga ambaye alimtaka Lissu kunyamaza kwa kuwa si mhusika ndipo wakaanza kurushiana maneno makali na kutaka kupigana huku kila mmoja akiwa ameshikiliwa na watu.
“Nitakufanya kama nilivyokufanya kule Singida na sijui kama umesahau... nitakushughulikia mimi si wa mchezo mchezo ,” alisema Wasonga huku akiwa ameshikwa na mawakili wanne.
Wakati huo, Lissu aliyekuwa ameshikwa mkono na Nyabiri alikuwa akirusha maneno kwa Wasonga akimweleza kuwa hawezi kumfanya kitu.
Kelele hizo zilimfanya Jaji Muhamed aliyekuwa akiendelea na kesi nyingine kuhoji sababu za kuwapo kelele nje hivyo kumtuma askari magereza ambaye aliwaambia jaji anahoji sababu ya kelele hizo.
Baada ya angalizo hilo, Nyabiri aliwasihi wanyamaze lakini Wasonga alionekana bado ana hasira hivyo mawakili wenzake kumtoa.
Nje ya mzozo huo, katika kesi mbili ambazo ziliwafikisha mahakamani hapo jana, Lissu ambaye ni mgombea urais wa TLS na mgombea umakamu wa rais, Godwin Ngwilimi walisema wanamwakilisha mgombea mwingine wa urais, Lawrence Masha kutaka mahakama ikubali ombi lao la kuingizwa katika kesi namba 12/2017 ambayo ilifunguliwa na Wasonga.
Katika kesi namba 12, Jaji Muhamed alianza kusoma barua ya Wasonga ya kutaka aiondoe mahakamani kwa kuwa ilifunguliwa kimakosa lakini akasema anayo hati ya kufungua upya baada ya marekebisho.
Alipomaliza kusoma barua hiyo, jaji akaomba muda wa kuitafakari huku akiwaomba mawakili wakubali kuhamisha chumba cha mahakama kutokana na idadi kubwa ya watu.
“Hii barua ya kuondoa kesi ndiyo nimeipata muda huu, naomba mnipe muda ili nitafakari, baada ya dakika 15 tukutane mahakama ya wazi maana hapa naona hapatoshi, lakini siyo lazima mje na majoho kwani mnajulikana,” alisema.
Baada ya dakika 20 wakiwa katika mahakama ya wazi, Jaji Muhamed aliwaita mawakili wa pande zote na kuzungumza nao kwa dakika 22 ndipo wakarejea saa 5:40 asubuhi. Kesi hiyo iliendelea tena huku kila upande ukipewa dakika sita ukianza na upande wa waliopeleka maombi ya kutaka waunganishwe katika kesi hiyo.
Mawakili hao; Lissu, Fred Kalonga, Paul Kaunda na Ngwilimi waliamua kumpa dakika zao Lissu na akazitumia kuwasilisha kile walichokiita hati ya haki.
Lissu alisema waliamua kuomba nafasi ya kuunganishwa katika kesi hiyo kwani wanajua kuwa kama hawataunganishwa, kwa vyovyote haki yao inaweza kupotea na hasa kwa wagombea.
“Mheshimiwa jaji, mimi Tundu Lissu na Lawrence Masha ni wagombea wa nafasi ya rais wa TLS, lakini pia yupo mwenzetu Godwin Ngwilimi ambaye anagombea nafasi ya makamu wa rais, kwa pamoja tunaomba kuunganishwa katika kesi hii kwa kuwa tuna masilahi na tunaweza kupoteza,” alisema Lissu na kuongeza:
“Kanuni ya 14 ya Mwenendo wa Mashtaka inaruhusu mtu mwenye masilahi kuomba aingizwe. Katika kanuni hiyo kifungu cha 1 na 2 vinaruhusu mheshimiwa Jaji, na hati ya maombi inajieleza yenyewe.”
Baada ya kueleza hayo ilikuja zamu ya Wasonga ambaye alisema, “Mheshimiwa Jaji, hakuna mahali ambapo mawakili hawa wanaweza kuingia na sheria inawaondolea uhalali hata wa kuleta maombi ya aina hii.”
0 comments:
Post a Comment