Waziri Mkuu Mstaafu ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa amejibu madai ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Abdallah Bulembo kuwa aliwahi kumsaidia shilingi milioni 40 za kampeni.
Bulembo ambaye pia ni Mbunge wa kuteuliwa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana aliliambia gazeti la Mwananchi kuwa aliwahi kuiomba kambi ya Lowassa kiasi cha shilingi milioni 40 ili zimsaidie katika kampeni za uchaguzi wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, mwaka 2014, kiasi ambacho anadai alipewa na kambi hiyo.
“Unajua kipindi kile nagombea uwenyekiti nilimfuata Lowassa nikaomba anichangie katika kampeni zangu, naye alinipa shilingi milioni 40,” Bulembo anakaririwa.
Alidai kuwa kambi hiyo iliutumia msaada huo kama fimbo wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais, baada ya kuona kuwa hamuungi mkono Lowassa kwani alikuwa akimuunga mkono Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda. Alisisitiza kuwa hakuwahi kuwa kambi ya Lowassa na kwamba baada ya kuona wanamzonga kwa kumuita msaliti, aliahidi kuuza gari zake mbili ili awarudishie kiasi hicho cha fedha alichopewa kama msaada. Lakini hakufanya hivyo.
Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda akizuzungumza na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania, Abdallah Majura Bulembo (kulia) na Makamu wake Dogo Idd Mabrouk
Hata hivyo, Lowassa alikanusha vikali madai hayo ya Bulembo akiyaita upuuzi usio na ukweli wowote.
“Sio kweli,” alisema Lowassa. “Huo ni upuuzi, upuuzi mtupu,” alisisitiza katika mahojiano yake na gazeti hilo kuhusu madai ya Bulembo.
0 comments:
Post a Comment