Friday 14 April 2017

Isome hapa: Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016.|Soma


Jana 13 Aprili, 2017 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Juma Assad aliwasilisha Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2016.
Akizungumza na waandishi wa habari alisema;

Ndugu wanahabari,

Kwa mwaka wa fedha unaoishia 30 Juni, 2016 nimefanya ukaguzi na kutoa ripoti kwa jumla ya Taasisi 543 ambazo ni; Taasisi za Serikali Kuu 222; Serikali za Mitaa 171; Mashirika ya Umma 150 kati ya 200. Katika Taasisi hizo pia, nimekagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kutoa ripoti 797.

MATOKEO YA UKAGUZI WA HESABU
Hati za Ukaguzi
Ndugu Wanahabari,
Katika ukaguzi wa Hesabu nilioufanya katika mwaka wa fedha 2015/2016 nimetoa jumla ya Hati 505, zinazohusu usahihi wa Hesabu zilizoandaliwa na mihimili mitatu ya dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama. Kati ya hizo, Hati zinazoridhisha ni 436 (86.34%); Hati zenye shaka ni 60 (11.88%); Hati zisizoridhisha ni nne (0.79%); na Hati Mbaya ni tano (0.99%).


USIMAMIZI WA MAPATO YATOKANAYO NA KODI
Ndugu Wanahabari,
Kwa mwaka ulioshia tarehe 30 Juni, 2016, makusanyo ya mapato yatokanayo na kodi yalipita malengo yaliyowekwa kwa asilimia 1, kutoka makisio ya shilingi bilioni 12,362.96 hadi kufikia makusanyo ya shilingi bilioni 12,509. Makusanyo hayo yanajumuisha misamaha ya kodi iliyotolewa kwa watumishi wa Umma kupitia manunuzi mbalimbali ya shilingi bilioni 25.69.8

USIMAMIZI WA DENI LA TAIFA
Ndugu Wanahabari,
Hali ya Deni la Taifa; Deni la Taifa kufikia tarehe 30 Juni, 2016 lilikuwa shilingi bilioni 41,039.39 [30 Juni 2015: bilioni 33,539.59] likiwa na ongezeko la bilioni 7,499.80 sawa na asilimia 22 ikilinganishwa na deni la mwaka uliopita. Aidha, kiasi hiki cha deni kilichoripoitiwa tarehe 30 Juni hakijajumlisha Shs. Bilioni 3,217 (sawa na 8% ya deni lililoripotiwa) ambayo ni madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii (TZS. 2,991.4 Billion) na madeni ambayo hayajalipwa na yanadhana ya Serikali (Expired Guarantees: TZS 225.6 Billion).

Hii inaashilia kuwa kiasi cha Deni la Taifa lililoripotiwa tarehe 30 Juni 2016 ni kidogo kuliko hali halisi. Ukaguzi imebaini kuwa Serikali imeshindwa kulijumuisha deni la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutokana na ucheleweshaji wa kutoa hati fungani (Non cash bond) ambazo Serikali iliahidi kuzitoa. Hivyo kukosekana kwa “instrument” inayomuwezesha Mhasibu Mkuu wa Serikali kuliingiza deni hili kwenye vitabu.

Aidha, Ukaguzi umebaini kuwa Deni la Taifa linakuwa kwa haraka kwa Zaidi ya asilimia 20, kwa mwaka ambayo kwa kiasi kikubwa kinatokana na mikopo ya biashara. Hivyo kusababisha marejesho ya deni na riba (debt service) kuongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na gharama za mikopo na muda mfupi wa urejeshwaji wake. Kwa kuangalia gharama za kuhudumia Deni la Taifa na kulinganishwa na mapato ya ndani, gharama hizo ziko juu ya viwango vinavyohitajika. Angalia Jedwali hapa chini linaloonyesha viashiria mbalimbali ya deni la taifa.

Matumizi yasiyokuwa na manufaa kwa Serikali Shilingi bilioni 2.02
Ukaguzi wangu umebaini matumizi yasiyokuwa na manufaa yenye jumla ya shilingi bilioni 1.46 kwa Serikali Kuu. Matumizi hayo yangeweza kuepukwa endapo Taasisi husika zingekuwa makini.Kwa upande wa Serikali za mitaa, Halmashauri 14 zililipa jumla ya shilingi milioni 564.94 kwa taasisi husika. Mfano wa malipo hayo ni tozo mbalimbali, riba na gharama za usumbufu zinazojitokeza kutokana na kesi au kutotimiza masharti ya mikataba. Sababu zingine ni malipo yanayolipwa mara mbili.
Naishauri Serikali kutekeleza majukumu yake ya mikataba ili kuepuka kufanya malipo yasiyokuwa na manufaa yoyote kwa Serikali. Pia, kuimarisha udhibiti wa ndani katika kutekeleza majukumu yake ili kuondokana na migogoro mbalimbali isiyo na tija.

USIMAMIZI WA MALI NA MADENI YA SERIKALI
Ndugu Wanahabari,
Uwepo wa Mali za kudumu zilizotelekezwa; Ukaguzi wangu umebaini ongezeko la idadi ya magari yaliyotelekezwa katika taasisi mbalimbali za Serikali Kuu kutoka magari 675 mwaka 2014/15 hadi kufikia magari 1,272 mwaka 2015/16 (sawa na ongezeko la asilimia 88).Kwa upande wa Serikali za Mitaa, jumla ya magari, pikipiki na mitambo inayofikia 652 yalitelekezwa pasipo hatua zozote kuchukuliwa na menejimenti. Aidha, kwa upande wa Idara na Wakala wa Serikali, jumla ya magari 92 yalitelekezwa. Hata hivyo, menejimenti ya Taasisi husika haikuchukua hatua yoyote. Uwepo wa mali hizi kwa muda mrefu pasipo kuuzwa, unaweza kusababisha hasara itokanayo na wizi wa vifaa na uchakavu.
Naishauri Serikali kuimarisha usimamizi wa mali za kudumu ili kuepusha uharibifu utokanao na kutelekezwa kwa mali hizo kwa muda mrefu.

Dawa zilizokwisha muda wa matumizi ambazo hazijaharibiwa Shilingi bilioni 10.19
Kwa kwa upande wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo, Uhakiki wa dawa zilizonunuliwa kupitia fedha za Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na Malaria, Ukimwi, na Kifua Kikuu uliofanyika kwenye ghala la Bohari Kuu ya Dawa umegundua uwepo wa dawa zilizokwisha muda wake zenye thamani ya Sh.10,187,671,563 ambazo ni mkusanyiko wa dawa hizo kwa miaka 12. Utunzaji wa dawa zilizokwisha muda wake kwa muda mrefu yanaongeza gharama za utunzaji.
Ninaishauri Serikali iharakishe uteketezwaji wa dawa zilizokwisha muda wake kuondolewa kwa wakati kuepusha gharama za utunzaji na athari zinazoweza kujitokeza.

MATOKEO YA UKAGUZI WA MASHIRIKA YA UMMA
Shirika la Usambazaji wa Umeme Tanzania (TANESCO); TANESCO ina malimbikizo makubwa ya madeni katika manunuzi ya umeme kutoka kwa watengenezaji huru wa nishati (IPPs) na Watengenezaji wa dharura wa nishati (EPPs).Hii imesababishwa na TANESCO kununua umeme kwa bei ya wastani wa Shilingi 544.65 kutoka kwa IPPs/EPPs na kuuza kwa wastani wa Shilingi 279.35 kwa kila uniti hivyo kusababisha hasara ya wastani wa Shilingi 265.30 kwa kila uniti.Jitihada zaidi zinahitajika kuliokoa Shirika katika hali liliyopo kwa kutafuta vyanzo mbadala vya umeme vyenye bei nafuu kama matumizi ya umeme unaozalishwa kwa maji na nishati ya gesi na kuachana na wazalishaji binafsi wanaotumia mafuta.

Hayo ni baadhi ya matokeo niliyokuwekea kuendelea kujua zaidi kilichomo kwenye ripoti hiyo soma hapo chini nimekuwekea.

Muhtasari wa matokeo ya Ukaguzi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2016. |Download Here|

0 comments:

Copyright © 2017 KwilasaNewsline | We Call Away| All Right Reserved|
Scroll To Top