Friday 14 April 2017

Askari 7 wa Jeshi la Polisi wauawa kwa kupigwa risasi wilayani Kibiti mkoani Pwani.|Soma

Askari 7 wa Jeshi la Polisi jana jioni waliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika walipokuwa wakilinda doria katika kijiji cha Jaribu wilayani Kibiti mkoani Pwani.

Askari hao walishambuliwa na watu wasiojulikana majira ya saa 12 jioni walipokuwa kwenye gari lao wakirejea kituoni Bugu baada ya kumaliza kuweka doria.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga alisema kuwa kwa sasa hawezi kuzungumzia tukio hilo kwani ni mapema sana. Aliwasihi waandishi kumuacha kwanza hadi hapo taarifa rasmi itakapoandaliwa ataweza kuujulisha umma kuhusu yale yote yaliyotokea.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo licha ya kusema kuwa hana taarifa za kutosha juu ya tukio zima hadi hapo atakapowasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Ernest Mangu. Lakini aliahidi kuwa, watu hao watatafutwa popote pale walipo na hatua dhidi yao zitachuliwa ili kukomesha vitendo hivyo.

Kwa mujibu wa taarifa za awali zinadai kuwa, dereva wa gari la polisi alipigwa risasi na kupoteza uwezo wa kuongoza gari na kisha askari wengine walikuwapo wakashambuliwa. Askari mmoja aliyejeruhiwa amelazwa katika Hospitali ya Mchukwi.

Hii si mara ya kwanza kwa matukio ya mauaji kutokea wilayani Kibiti, kwani kwa siku za nyuma viongozi wa serikali wamekuwa wakiuawa na watu wasiojulikana jambo ambalo linazidi kuzua hofu kwa wakazi wa eneo hilo.

Tukio la mwisho kutokea wilayani humo lilikuwa ni Machi mwaka huu ambapo polisi waliwaua watu watatu karibu na Daraja la Mkapa waliokuwa wamevalia baibui wakati ni wanaume huku wakiendesha pikipiki baada ya kukaidi agizo la kusimama.

0 comments:

Copyright © 2017 KwilasaNewsline | We Call Away| All Right Reserved|
Scroll To Top