Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 16 Machi, 2017 ametembelea eneo la ujenzi wa Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma na kuwahakikishia wananchi kuwaatahamia Dodoma hivi karibuni kama alivyoahidi.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenister Joakim Mhagama na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amesema pamoja na majengo ya Ikulu Serikali itajenga miundombinu mingine zikiwemo reli na barabara za lami zitakazounganisha maeneo ya vijiji vinavyozunguka Ikulu na mji wa Serikali.
Pia Mhe. Dkt. Magufuli amewahakikishia wananchi kuwa wote watakaoguswa na shughuli za ujenzi wa miundombinu ya Serikali na wanaostahili kulipwa fidia watalipwa, na ametoa wito kwa wananchi hao kutumia fedha za fidia watakazolipwa kujenga makazi bora na kujipanga kufanya shughuli zenye manufaa kwao.
“Hapa sasa watakuja watu wengi, wafanyakazi na wageni maana tayari Mabalozi wa nchi mbalimbali nao watajenga ofisi zao hapa, sasa na nyinyi mjipange kufanya biashara, mtapata soko la kuuza mazao na bidhaa nyingine, mkipata fedha ziwasaidie kwa manufaa na sio kuzichezea” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
0 comments:
Post a Comment