Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limefikia makubaliano na Kampuni ya Dangote Group of Industries kuhusu bei ya mauzo ya gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya kiwanda chake cha saruji kilichopo mkoani Mtwara.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Kapulya Musomba alisema makubaliano hayo yanahusu kuunganisha miundombinu ya kusafirisha gesi asilia kutoka kwenye bomba kubwa kwenda kiwandani hapo na kukamilisha mkataba wa awali kwa ajili ya mauzo ya gesi kwa matumizi ya kiwanda hicho.
Alisema makubaliano hayo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli. Desemba mwaka jana, Rais Magufuli alipokutana na mmiliki wa kiwanda hicho, Aliko Dangote jijini hapa alimtaka kununua gesi moja kwa moja kutoka TPDC badala ya kutumia watu wa kati wenye nia ya kutengeneza faida binafsi.
Mwakilishi wa Kampuni ya Dangote, Sada Ladan-Baki alisema gharama za kuunganisha bomba hadi kiwandani zitabebwa na kampuni hiyo na siyo Serikali ya Tanzania.
“Tutagharamia ujenzi wa bomba, mwanzo hadi mwisho na tutaanza ujenzi mwezi ujao,’’ alisema.
0 comments:
Post a Comment