Serikali: Imezipaga marufuku shule binafsi kufukuza wanafunzi wanaofeli wastani.|Soma
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezitaka shule zote zilizowataka wazazi/walezi kuwahamisha watoto wao kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu, kufuta agizo hilo na kuendelea na wanafunzi hao bila masharti yoyote.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kaimu Kamishna wa Elimu, Nicolas Buretta imeeleza kuwa wazazi wenye wanafunzi waliorudishwa nyumbani kwa sababu hiyo wahakikishe wanawarudisha kwenye shule walizokuwa wakisoma ili waendelee na masomo yao kama kawaida.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali imefikia hatua hiyo baada ya kubainika kuwa bado kuna shule nyingi za msingi na sekondari hususani zisizo za Serikali na zaidi za kidini zinazoendelea kukaririsha, kuhamishia shule nyingine au kuwafukuza wanafunzi kwa kigezo cha kutofikia alama za ufaulu zilizowekwa na shule hizo jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Badala ya shule hizo kuchukua hatua hiyo, wizara hiyo imesema, “...Ziwe na utaratibu wa kuinua viwango vya taaluma kwa wanafunzi wenye ufaulu mdogo na hivyo siyo ruhusa kukaririsha darasa wanafunzi kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu uliowekwa na shule. Ikitokea, ni lazima kufanya hivyo, taratibu zilizopo zifuatwe.”
Taarifa hiyo imeelekeza wadhibiti ubora wa shule, kanda na wilaya, maofisa elimu wa mikoa na wilaya kusimamia utekelezaji wa agizo hilo katika maeneo yao.
“Shule yoyote itakayokiuka maagizo hayo itachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria zilizopo.”
Akizungumzia agizo hilo la Serikali, Katibu wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania, (Tamongsco), Benjamin Nkonya amesema wanachama wake hawafukuzi wanafunzi baada ya kushindwa vigezo bali, inaangalia uwezo wake wa kujifunza mambo mawili; ung’amuzi wa kujifunza kwa nadharia na ufundi au mchindo.
“Tukiona mwanafunzi amefeli katika ung’amuzi, mfumo ambao Serikali inauzungumzia, tunampeleka katika mchindo ambao ni ufundi stadi na siyo kuwarudisha nyumbani,” amesema Nkonya.
Amefafanua kwamba, mchindo ni kama chuo cha Veta ambacho dereva asiyejua kusoma na kuandika anakwenda kujifunza na mwishowe anakuwa dereva bora.
Amesema mfumo huo unasaidia kukuza wabunifu hasa katika mapinduzi ya Serikali kuwa nchi ya viwanda.
Hatahivyo, Waziri Kivuli wa Elimu, Suzan Lyimo amesema kinachofanyika kwa mujibu wa agizo hilo ni Serikali kutaka shule za Serikali na binafsi ziwe na mfumo wa utoaji elimu unaofanana jambo ambalo ni gumu.
Ameitaka Serikali iunde mamlaka ya kudhibiti huduma za utoaji wa elimu ili ijiondoe katika usimamizi wa moja kwa moja katika uendeshaji wa sekta hiyo.
0 comments:
Post a Comment