Lowassa kwa Mara nyingine tena Bungeni, Wabunge wa charukiana
Edward Lowassa bado angali vinywani mwa wabunge japokuwa hayupo tena Bungeni . Jina lake jana limeibua mjadala bungeni wakati wabunge walipotoleana maneno makali kuhusu waziri huyo mkuu wa zamani.
Sakata hilo limetokea wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipokuwa likijadili Muswada wa Huduma ya Habari ambao ulipitishwa jana licha ya kupingwa vikali na kambi ya upinzani na wadau wa habari.
Jina la Lowassa lilizua tafrani bungeni baada ya wabunge wawili kurushiana maneno kuhusu taarifa zake tofauti zilizokuwa zikiandikwa na vyombo vya habari kiasi cha kusababisha mwenyekiti wa Bunge aingilie kati.
Akichangia muswada huo, mbunge wa viti maalumu (CCM), Amina Mollel amerejea sakata la zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura iliyopewa kampuni ya Richmond Development ya Marekani ambayo ilibainika baadaye kuwa haikuwa na uwezo. Sakata hilo lilitokea wakati Lowassa akiwa Waziri Mkuu.
“Mimi naomba ninukuu baadhi ya vichwa vya habari ambavyo vilitumiwa katika magazeti,” amesema Mollel, ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari.
Mollel ametaja mfano wa gazeti lililoandika “Lowassa anajua uzalendo au ni machozi ya mamba” na kichwa kingine cha habari cha gazeti hilo kilichosema “Lowassa Hasafishiki” na kingine kilichosema “Lowassa karibu Chadema”.
“Kuna haja ya kuwa na waandishi ambao leo hii wanaandika habari kwamba mtu huyo ni mbaya lakini kesho hiyo hiyo uongo huo unabadilika na kuwa ukweli?” amehoji Mollel.
Amesema Taifa linahitaji kuwa na sheria kama hiyo ambayo inaweza kulinda taaluma ya waandishi wa habari, hivyo kupitishwa muswada huo ni kwa manufaa ya wanahabari.
Maneno hayo kuhusu Lowassa yakamfanya mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji kusimama na kutumia methali inayosema “ukienda kwa wenye chongo, ufumbe macho ili ufanane nao japokuwa unaona”.
“Leo kituko cha karne hii ni pale anaponyanyuka mbunge wa CCM ndani ya Bunge akatulaumu eti sisi (wabunge wa kambi ya upinzani) kwa sababu tunampenda Lowassa. Hiki ni kituko cha karne,” amesema.
“Rudini kwenye kumbukumbu ya Mkutano Mkuu wa CCM kuhusu kale kawimbo katamu. Kweli?” amesema na kufanya wabunge wengine wa upinzani kuanza na kuimba “tuna imani na Lowassa”.
Jina la Lowassa limekuwa likiibuka kwenye vikao mbalimbali na katikati ya mwaka lilikuwa gumzo kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM ulioitishwa kwa ajili ya uchaguzi wa mwenyekiti mpya wa chama hicho.
0 comments:
Post a Comment