Katika toleo namba 387 la Jumatatu April 17-23, 2017 gazeti la MwanaHalisi katika ukurasa wake wa kwanza lina habari isemayo:“Mwakyembe: Maisha Yangu Yako Hatarini.”
Habari hiyo inadai kuwa Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo hayuko huru na maisha yake bado yapo hatarini, taarifa ambayo imemshtua na kumhuzunisha sana Waziri kwa uzushi, ulaghai na uzandiki uliopitiliza.
Mwandishi wa habari hiyo amedai kufanya mahojiano na Dkt. Mwakyembe nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma Alhamisi iliyopita, na amenukuu kile anachodai ni Waziri kueleza wasiwasi kuhusu usalama wa maisha yake, kitu ambacho hakikutokea.
Tunapenda kuutaarifu umma kuwa, habari hiyo ni ya uongo na ya kutunga. Mhe. Dkt. Mwakyembe hajafanya mahojiano yoyote na mwandishi yeyote katika siku na mahali palipotajwa sembuse mwandishi husika wa gazeti la MwanaHalisi ambalo Mhe. Mwakyembe ana kesi nalo Mahakama Kuu kwa kumzushia habari za uongo alipokuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Wakati Serikali ikitafakari hatua za kuchukua kwa uandishi wa aina hii, tasnia ya habari inaendelea kukumbushwa kuzingatia weledi na maadili hasa wakati huu ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya 2016, tasnia ya habari imepewa hadhi ya kuwa taaluma kamili.
0 comments:
Post a Comment