Monday, 7 November 2016

Rais Magufuli ametuma Salamu za Rambirambi Kufuatia Kifo cha Spika Mstaafu Mhe. Samwel Sitta.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai kufuatia kifo cha Spika Mstaafu na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Urambo lililopo Mkoani Tabora Mhe. Samwel Sitta.

 

Mhe. Samwel Sitta amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani alikokuwa akipatiwa matibabu tangu mwezi uliopita.

 

Katika salamu hizo, Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mhe. Samwel Sitta na kwamba Taifa limempoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo.

 

“Nitamkumbuka Mzee Sitta kwa uchapakazi wake, uzalendo wake na tabia yake ya kusimamia ukweli katika kipindi chote alichokuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali za siasa na Serikali.

 

“Kupitia kwako Mhe. Spika naomba kutoa pole nyingi kwa Mke wa Marehemu Mhe. Magreth Sitta ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Urambo na familia nzima ya marehemu, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wananchi wa Urambo Mkoani Tabora na watu wote walioguswa na msiba huu” amesema Rais Magufuli katika salamu hizo.

 

Dkt. Magufuli amesema anaungana na wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na amewaombea moyo wa uvumilivu na ustahimilivu.

 

“Namuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu mahali pema peponi, Ameni”

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

07 Novemba, 2016

-------------------------------------------------------------------------------------------------------

 
Spika wa Bunge Mstaafu, Samuel Sitta (74) amefariki dunia usiku wa kuamkia leo wakati akipatiwa matibabu nchini Ujerumani.


Mtoto wa marehemu, Benjamin Sitta amesema baba yake amefariki saa 10:00 usiku wa kuamkia leo.


‘’Nikweli mzee amefariki nchini Ujerumani akiwa anapatiwa matibabu, alipelekwa Alhamisi iliyopita na alikuwa anasumbulia na saratani ya tezi dume ambayo ilisambaa na kuathiri miguu na mwili mzima."


Benjamin amesema kuwa taarifa za mipango ya kusafirisha mwili zitatolewa baadaye.

 
Sitta alikuwa Spika wa Bunge tangu mwaka 2005 hadi mwaka 2010 na pia mbunge wa Urambo Mashariki.


Pia, alikuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba na aliwahi kuwa waziri katika wizara mbalimbali kwa vipindi tofauti.


Alikuwa miongoni mwa wanachama zaidi ya 42 wa CCM waliochukua fomu za kugombea urais mwaka jana.

0 comments:

Copyright © 2017 KwilasaNewsline | We Call Away| All Right Reserved|
Scroll To Top